Fumo, Waridi na Shaka wakawa mguu niponye! Walikimbia kwa kasi ya farasi wa mashindano na wala hawakutazama nyuma. Walikimbia mpaka shuleni walikokutana hapo awali.

“Duh, Mzee Pilipili ni mkali kama jina lake .” Waridi alisema.

“Naam, ni mkali sana. Lakini mimi naona anaficha jambo kumhusu Rehema. Ninamshuku sana Mzee Pilipili.” Fumo alisema.

“Mimi nahisi Rehema yuko hatarini, ila sijui ni hatari gani lakini moyoni mwangu nahisi yuko hatarini na tunahitaji kufanya jambo ili tumuokoe.” Shaka alisema.

“Lakini hadi sasa hatuna ushahidi wa jambo lolote na baba yake ametufukuza kama kuku. Ni kweli pafukapo moshi hapakosi moto. Hapa kuna jambo ni lazima tulijue.” Waridi aliongeza.

“Hamjambo Fumo, Waridi na Shaka?” Msichana mmoja aliwasalimu.

“Hatujambo.” Fumo, Shaka na Waridi walimjibu kwa sauti huku wakishangaa jinsi yule msichana ambaye hawakumfahamualiyajua majina yao.

Msichana yule alijiunga nao na kuwaeleza.

“Msishtuke, . mimi ni binamu ya Rehema na niliwaona mlipokuwa pale nyumbani na hata mlipofukuzwa na ami yangu, Mzee Pilipili.” Msichana yule alisema.

Fumo, Shaka na Waridi walifurahi sana kukutana na jamaa ya Rehema. Wakaona huenda wakapata ukweli kuhusu aliko Rehema.

“Tumefurahi sana kukujua. Je, unaitwa nani?” Fumo alimuuliza binamu ya Rehema.

“Jina langu ni LuluNiliona mlivyofukuzwa na ami yangu . Poleni sana. Nimetumwa na Rehema niwaeleze jambo muhimu sana.” Lulu aliongeza.

“Umetumwa na Rehema, yuko wapi?” Shaka alirusha swali upesi kama risasi.

Kabla hajasema kitu walimuona Mzee Pilipili akikimbia kuelekea kule walikokuwa wamesimama, wote wanne waligutuka na kutimua mbio kuelekea kwa kina Fumo

“Huyu ami yako bado anatufuata ? ” Fumo alisema walipokaribia nyumbani kwao.

“Naam ami yangu ni mkali lakini kuna jambo muhimu nitawaeleza .” Lulu alisema huku akihema kwa sababu ya kukimbia.

“Sasa tueleze, Rehema yuko wapi na amesema utueleze nini? Kwa nini haji shuleni?” Fumo alimrushia Lulu maswali mengi.

“Kuna jambo baya ambalo litamfanyikia Rehema kesho. Rehema anatusihi tuchukue hatua ya haraka tumwokoe kutokana na jambo hilo.” Lulu alisema huku akiwatazama Fumo na wenzake.

“Rehema yuko wapi? Ni jambo gani hili?” Fumo aliuliza akiwa na wasiwasi mwingi.

“ Rehema yuko nyumbani amefichwa asionekane . Baba yake amemficha kwa muda wa wiki mbili sasa. Amemkataza asiende shuleni kwa sababu ya jambo kubwa litakalotokea kesho.” Lulu alisema.

“Hili ni jambo gani? Tueleze tujue la kufanya sasa hivi kumwokoa mwenzetu.” Waridi alisema.

“Rehema anaozwa kwa nguvu kesho. Anaozwa kwa Mzee Mapengo ambaye ni babu tajiri kutoka mji wa Tatu. Ami yangu Mzee Pilipili ameamua kumwoza Rehema ili apate mali na awe tajiri. Kwa hivyo kesho kutakuwa na harusi ya siri ambapo Mzee Mapengo atamwoa Rehema.” Lulu alisema huku wenzake wakibaki kuduwaa kwa mshtuko.

“Kwa nini Mzee Pilipili amwoze msichana mdogo kama Rehema kwa jizee lile? Ndoa ya mapema ni kinyume cha sheria.” Waridi alisema kwa kero.

“Rehema amenituma niwaeleze kuwa tufanye bidii ili tumwokoe kabla hajaolewa na huyo mzee kwani yeye anataka kuendelea na masomo yake.” Lulu alisema huku akiwatazama kina Fumo.

“Sasa tutafanya nini?” Shaka aliwauliza wenzake.

“Naona twende tumweleze baba yangu haya yote” Fumo aliwaambia wenzake, kwani baba yake alikuwa polisi.

Je, ungefanya nini kama jambo kama hilo lingemfanyikia rafiki yako?