Jumamosi asubuhi, Fumo, Shaka na Waridi walikutana shuleni kama walivyokubaliana. Kisha wakashika njia guu mosi guu pili hadi nyumbani kwa kina Rehema. Walifika na kubisha mlango. Mlango ulifunguliwa na mama yake Rehema ambaye aliwatazama kwa uso wa huzuni . Watoto walipomuona mama yake Rehema walipumua na hofu yao ikapungua. Wao waliogopa kukumbana na baba yake Rehema. Mama yake Rehema alionekana mwanamke mpole ijapokuwa alijawa hofu nyingi usoni.

“Karibuni wanangu.” Mama yake Rehema aliwakaribisha Fumo, Shaka na Waridi. Watoto wote waliingia nyumbani na kuketi kwenye makochi sebuleni. Aliwadadisi watoto wale na kusema.

“Kabla mniambie lolote, subirini niwaandalie chai mnywe halafu tuongee.” Mama yake Rehema alisimama na kwenda jikoni na kuwaacha watoto peke yao sebuleni . Baada ya muda, Mama ya Rehema alirudi na kuwapa watoto chai na biskuti . Fumo, Shaka na Waridi wakanywa chai. Baada ya kurudisha vyombo jikoni, mama ya Rehema alirudi sebuleni na kuketi na watoto wale.

“Haya nielezeni wanangu, ni jambo gani lililowaleta kwetu leo?” aliwauliza huku akitabasamu kuficha hofu aliyokuwa nayo.

“ Tumekuja kumjulia hali Rehema.” Waridi alisema.

“Wiki mbili zimepita sasa hatujamuona shuleni. Tukaamua tuje tumjulie hali na tujue kuna nini kilichosababisha asije shuleni?” Fumo akajaliza.

“Rehema yuko wapi? Tunaomba kumuona.” Shaka aliongeza.

Mama Rehema hakuwajibu aliwatazama wakimuuliza maswali yaliyofuatana kama polisi. Alisubiri wamalize kuongea, ndipo alipoafungua mdomo na kuzungumza.

“Wanangu, Rehema mwenzenu ana…” Kabla ya kumaliza kuzungumza, Mzee Pilipili, baba yake Rehemaaliingia ghafla na mama Rehema akakata uneni.

“Hawa watoto wana ninina wanatafuta nini kwangu?” Mzee Pilipili alimuuliza mkewe kwa sauti ya mgurumo kama simba huku akiwaonyesha kina Fumo kwa kidole.

“Wamekuja tu kututembelea na kumtafuta rafiki yao Rehema.” Mama yake Rehema alijaribu kumpoza Mzee Pilipili ambaye alikuwa akihema kwa hasira za moto wa kifuu kama mwanandondi ambaye alikuwa tayari kuingia kwenye ulingo wa ngumi.

“Baba shikamoo. Sisi hatuna ubaya tumekuja kumjulia hali Rehema kwani hatujamuona kwa muda wa wiki mbili sasa. ” Fumo alisema kwa unyenyekevu huku akimtazama Mzee Pilipili.

“Naam, tumekuja kumjulia hali mwenzetu Rehema kwani tumempeza sana na hatujui kama ni mgonjwa au amepatwa na jambo gani?” Waridi aliongezea.

“Basi nisikilizeni kwa makini nyinyi watoto! Rehema hayuko hapa! Nataka nyote mwondoke na mrudi kwenu kama hamtaki shida!” Mzee Pilipili alifoka.

“Lakini tumekuja kumjulia hali Rehema tu…” Shaka alianza kusema.,lakini kabla ya kumaliza Mzee Pilipili aliingia chumbani na kutoka na fimbo kubwa. Alivyoushika, watoto wale walijua kuwa wangechapwa . Wote watatu walitoka mbio na kuelekea barabarani huku Mzee Pilipili akiteta na kuwarushia maneno makali!

Je, unafikiri kwa nini Mzee Pilipili anafanya aliyoyafanya?