Fumo na wenzake walikuwa darasani. Mwalimu Beka alikuwa akiwafunza somo la Hesabu. Wanafunzi wote walikuwa wametulia wakimsikiliza Mwalimu Beka. Fumo ndiye aliyekuwa na wasiwasi mwingi . Aligeukageuka kutazama dawati ambalo halikuwa na mwanafunzi lililokuwa nyuma yake. Dawati lile lilikuwa la mwanafunzi mwenzao Rehema. Mwalimu alipokuwa akifundisha akili ya Fumo ilitembea na kutoka darasani hadi mwalimu akamgundua.

“Fumo hebu jibu hilo swali?” Fumo aligutushwa kutoka kwenye luja ya fikra na Mwalimu Beka. Hakujua mwalimu alisema nini akabaki akimtazama tu huku amekodoa macho.

“Fumo naona hauko nasi darasani.” Mwalimu Beka alimwambia.

“Samahani mwalimu.” Fumo alisema.

“Je, kuna jambo linalokusumbua ?” Mwalimu alimuuliza .

Fumo alitikisa kichwa na kukanusha naye mwalimu aliendelea kufundisha . Mara, kengele ya kunywa chai ililia na wanafunzi wote walitoka darasani na kuelekea kwenye jumba la maakuli. Fumo alitembea na rafiki yake Shaka.
“Shaka, kuna jambo linalonisumbua ” Fumo alimwambia Shaka kwa sauti yenye mashaka.

“Jambo gani hilo Fumo?” Shaka alimuuliza huku akimtazama mwenzake kwa makini.

“Hii ni wiki ya pili sasa Rehema hajakuja shuleni. Je, unajua ana shida gani?” Fumo alimuuliza Shaka.

“Duh! Ni kweli kabisa, pengine tumuulize Waridi rafiki yake wa chanda na pete.” Shaka alisema.

Fumo na Shaka walifika kwenye jumba la maakuli na wakanywa chai pamoja na wenzao. Wakati walipokuwa wakinywa chai, Fumo alimuona Waridi kwa umbali na akamfuata ili amuulize maswali aliyokuwa nayo akilini.

“Je unajua kuwa rafiki yako Rehema hajakuja shuleni kwa muda wa wiki mbili sasa?” Fumo alimuuliza Waridi.

“Ni kweli, mimi ni jirani yake lakini sijamuona popote wala kokote ni kama alipotea ghafla bila kuonekana.” Waridi alisema.

“Je, ulifika kwao na kuwauliza wazazi wake?” Fumo alimuuliza Waridi.

“Naam, nilifika lakini hawakunipa jibu. Walinisindikiza kwa macho makali tu bila kusema lolote.” Waridi alisema.

“Ulienda lini?” Fumo alimrushia swali tena.

“Nilifika kwao siku ya Jumamosi.” Waridi alimjibu.

Fumo alimuacha Waridi na kutoka nje ya jumba la maakuli akiwa amegubikwa na fikira nyingi kumhusu Rehema. Alijiuliza maswali mengi sana ambayo hakupata majibu. Rehema ameenda wapi? Je, ameaga dunia? Lakini kama angekuwa ameaga dunia, tungejua kwani wazazi wake wangekuja kusema shuleni. Je, ni mgonjwa? Lakini kama ni mgonjwa mbona Waridi hakupata nafasi ya kumuona? Mbona alipotea tu ghafla na haijulikani aliko? Kwani alipelekwa wapi?
Fumo alipokuwa akiwaza, Shaka alimjia na wakaketi wote kuota jua.

“Nakuona bado una fikira nyingi kumhusu Rehema” Shaka alisema.

“Naam, nataka kujua Rehema ameenda wapi.” Fumo alimjibu.

“Kwa hivyo unaona tufanyaje?” Shaka alimuuliza Fumo. Kabla Fumo hajamjibu, Waridi alijiunga nao ili asikilize wanalopanga.

“Fumo tueleze unaona tufanyaje ndipo tujue Rehema aliko?” Waridi aliongeza.

“Naona twende sote watatu nyumbani kwa kina Rehema tumtafute na tujue aliko. Huenda anahitaji msaada wetu nasi tumetulia tu tukisoma bila wasiwasi.” Fumo aliwajibu wenzake.

“Baba yake ni mkali sana.” Waridi aliwakanya wenzake.

“Hata kama ni mkali twendeni tu . Tukifika tutawauliza jamaa zake watueleze aliko Rehema kisha tutaelewa kwa nini amekosa kuja shuleni kwa wiki mbili mfululizo.” Fumo aliongeza.

“Naam, mimi nakubaliana nawe mia fil mia. Kesho ni Jumamosi tukutane asubuhi hapa shueni ili twende tumtafute Rehema.” Shaka alikubaliana.

“Na tukimpata baba yake tumwambia kuwa tumemkosa rafiki yetu kwa muda wa wiki mbili na jambo hilo limetutia wasiwasi tumeona tumtafute ili tumjulie hali.” Waridi alisema.

Fumo, Shaka na Waridi waliendelea kuzungumza wakipanga mipango ya kuwatembelea jamaa za Rehema . Kengele ililia na wote wakakimbia kwenda darasani kuendelea na masomo ya siku ile.

Fumo aliporudi darasani alikuwa ametulia na wasiwasi ulikuwa umemtoka . Aliwasikiliza walimu wake huku akitabasamu.

Je unafikiri Rehema amepatwa na jambo gani?