Neo, Josh na Hope walikuwa wote kwa nyumba ya Gogo. Walikuwa wanaongea na kucheka kwa sauti.

“Shhhh!” Gogo alisema. “Siwezi kusikia kile wanachosema kwenye redio. Kujeni, hebu sisi sote tusikize kipindi ninachokipenda zaidi.”

Kila mtu alinyamaza na kusikiliza. Kwa ghafla, walisikia mtangazaji akitaja jina la bustani yao.

“Ala! Bustani yetu inajulikana sana!” Neo alsiema.

“… na Tiniso, anayejulikana pia kama Tin, atakuwa na maonyesho kwenye bustani hiyo jioni hii akiwa na bendi la We Can Band. Wasanii kutoka Zimbabwe, Nigeria na Malawi wataburudisha kwenye jukwaa. Kila mtu anakaribishwa kwenye tafrija hiyo!” mtangazaji alisema.

“Gogo,” Neo alisema, “umesikia matangazo hayo? Wamesema kila mtu anakaribishwa. Tafadhali tuhudhurie tafrija hiyo? Tafadhali?”

Gogo alimwangalia Neo na kutabasamu. “Ikiwa Josh na Hope wataruhusiwa kuhudhuria, basi mnaweza kuhudhuria pia,” alisema. Josh na Hope waliondoka upesi kuenda kuomba wazazi wao ruhusa wahudhurie tafrija kwenye bustani.

Waliporudi kumchukua Neo, Hope alimwambia Gogo kuwa Bella na mamake wangehudhuria tafrija hiyo pia.

“Sawa, mhudhurie basi. Mkae pamoja mkiwa huko,” Gogo alisema.

Kwenye bustani, Neo alimuona Bella na mamake, na hata Noodle alikuwa amekuja na wao. “Nafikiri kila mtu kutoka eneo letu yuko hapa,” Neo alisema. “Na baadhi ya wageni pia.”

“Sikiliza…” Josh alisema. “Kuna watu wanaozungumza Kifaransa?”

“Ndiyo!” Hope alisema. “Naweza kusikia lugha ya Chichewa na Shona pia.”

Neo alishika mkono wa Hope. “Tazama,” Neo alisema, “Msanii Tin anaburudisha jukwaani! Lakini wapi bendi la We Can Band?”

Hata kabla Hope aweze kujibu, Tin alikaribia kwenye mikrofoni. “Hamjambo!” Tin alisema. “JE, MKO TAYARI KUANZA TAFRIJA HII?”

“Yebo, ndiyo!” umati ulijibu kwa sauti.

Tin alianza kucheza gitaa yake. “Rudia ninayosema,” alisema huku akianza kuimba. “Mguu wa kushoto nyuma.”