Fumo aliwaeleza wenzake kuwa siku ya pili wakutane mapema ili wapange namna ya kumwokoa Rehema kutoka kwenye ndoa ya lazima. Jumapili asubuhi Waridi na Shaka walifika kwa kina Fumo saa kumi na mbili wakaketi nje wakiongea.
“Sasa tutampa ushahidi gani baba yangu ili atusaidie kumwokoa Rehema?” Fumo aliwauliza wenzake.

Wote walitafakari kwa makini lakini hawakupata jibu. Wakati walipokuwa wakiongea , walimwona Lulu akija mbio kama ambaye anafukuzwa. Alipowafikia aliinama huku akihema sana.

“Lulu kuna nini? Tueleze upesi.” Fumo alimuuliza.

“Jana mlipokuja na baba yako, Rehema alipewa dawa za kulala ili asiongee nanyi na pia dawa nyingi zikawekwa mezani kando ya kitanda ili mfikiri kuwa yeye ni mgonjwa. Rehema si mgonjwa hata kidogo. Pia nimejua pahali harusi itafanyika. Wataifanya kisiri katikati ya msitu wa Majanga. Tayari Rehema amepelekwa huko msituni na harusi itaanza wakati wowote. Hatuna muda sasa njooni tumwokoe.” Lulu alimaliza kisha akatimua mbio akarudi kwao ili asionekane akiongea nao.

Fumo aliingia nyumbani kwao mbio akamuamsha baba yake.

“Baba tafadhali amka. Ushahidi ulioutaka tuko nao sasa!” Fumo alisema kwa sauti kubwa huku akigongagonga mlango wa chumba cha kulala cha baba yake.

Inspekta aliamka na kuvaa sare yake na kutia bastola yake kiunoni. Aliketi na Fumo, Waridi na Shaka sebuleni.
“Mmepata ushahidi gani? Hebu nielezeni ndipo nichukue hatua ya upesi.” Aliwauliza watoto.

“Lulu ametueleza kuwa harusi inafanyika kisiri katikati ya msitu wa Majanga. Tayari Rehema amepelekwa huko na baba yake na wakati wowote harusi itafanyika .” Fumo alimjibu baba yake.

“Je mnamuamini Lulu?” Inspekta aliwauliza.

“Naam, Lulu hawezi kutudanganya kwa jambo kama hilo. Yeye pia anataka tumwokoe Rehema.” Fumo alimjibu .
“Sawa basi.” Inspekta alijibu kisha akachukua simu yake na kuwapigia mwenzake.

“Hello Koplo Popa. Njoo upesi pamoja na wenzako watano kwa gari la polisi! Kuna mzee anayetaka kumwoza mtoto wake mdogo msituni!” Inspekta aliongea kwa simu kisha akaikata na wote wakasubiri.

Ghafla bin vuu gari la polisi aina ya landrover lilifika likiwa na askari watano.

“Watoto mko tayari?” Inspekta aliwauliza Fumo, Waridi na Shaka.

“Tuko tayari Inspekta!” Wote walimjibu.

“Haya pandeni hapo nyuma twende msituni.” Inspekta aliwaambia.

Fumo, Waridi na Shaka walipanda nyuma ya gari wakaketi na wale polisi watano waliokuwa wamejihami na bunduki kubwakubwa. Inspekta aliketi mbele na dereva kisha gari likaondoka kwa kasi kuelekea msitu wa Majanga.

Gari lilifika msituni na kufuata kijia kilichokuwa mle msituni Walipofika sehemu ambapo hakukuwa na njia ya kupitia kwa gari, walishuka. Inspekta aliwaamuru wale askari wenzake na watoto watembee pamoja kwenda katika eneo la tukio.

Wote walitembea kwa kunyatianyatia msituni. Wale askari walikuwa wameshika bunduki zao tayari kufyatua risasi endapo hatari yoyote ingetokea. Inspekta alikuwa mbele akiwaelekeza kwa ishara za uso na mikono. Watoto nao walikuwa nyuma ya wale askari.

Waliona uwanja mdogo katikati ya msituni. Inspekta, askari na watoto walijificha kwenye vichaka na kutazama pale uwanjani. Uwanjani, waliona kuwa sherehe ya harusi ilikuwa karibu kuanza. Kwa umbali walimwona Rehema ambaye alikuwa anatokwa machozi njia mbilimbili akiwa amelazimishwa kusimama karibu na Mzee Mapengo.

Rehema alikuwa amevalishwa rinda la bi harusi naye Mzee Mapengo alikuwa amevalia suti maridadi. Mzee Mapengo alikuwa amefurahi Naye Mzee Pilipili alisimama kando ya Rehema. Vilevile walimwona muozaji ambaye alikuwa msimamizi wa harusi. Alikuwa mzee msimamizi wa mila na tamaduni. Mzee yule alikuwa amevaa nguo za kitamaduni. Mkononi alikuwa ameshika mkia wa ng’ombe kama mganga. Kulikuwa na wazee wengine wanne tu ambao walikuwa wamehudhuria ile harusi,nao walikuwa wamesimama kando kidogo kutazama sherehe.

Fumo, Waridi na Shaka walipomwona Rehema akitokwa na machozi, walisikitika sana. Mara wakamsikia yule mzee wa mila akiongea.

“Sasa ni wakati wa kufunga ndoa! Je Mzee Mapengo umekubali kumwoa Rehema Pilipili kama mkeo…” Kabla mzee yule kumaliza usemi, Inspekta alitoa amri askari wake wasonge mbele na wawatie mbaroni wote waliohudhuria ile harusi .
Askari waliruka na bunduki zao huku watoto wakiwafuata nyuma. Mzee Pilipili alipowaonaona Inspekta na polisi wenzake alijaribu kutoroka lakini polisi mmoja alikimbia na kumkamata.

“Mzee Pilipili na wenzako, leo tunawakamata kwa hatia ya kujaribu kumwoza mtoto mdogo. Nyote muwe tayari kufungwa jela kwa muda mrefu mkifika kortini kesho!” Inspekta alisema huku yeye na wenzake wakiwafunga pingu wote waliohudhuria harusi ile. Fumo, Waridi na Shaka walikimbia na kumkumbatia huku wakiwa na tabasamu
“Asanteni sana marafiki zangu. Marafiki wa kweli hujulikana wakati wa shida. Leo mmeniokoa kutoka kwenye kinywa cha mamba.” Rehema alisema huku akitokwa na machozi ya furaha.