Baada ya kuwaeleza kina Fumo kila kitu kuhusu masaibu ya Rehema, Lulu alikimbia na kurudi kwao. Aliwaahidi Fumo kuwa akijua pahali ambapo harusi itafanywa atarudi kuwambia.

Fumo, Shaka na Waridi waliingia nyumbani kwa kina Fumowakampata Inspekta akiwa amevalia sare yake ya polisi Alikuwa anajitayarisha kwenda katika kituo cha polisi kuendelea na kazi yake.

“Aaah wanangu karibuni . Fumo, leo umekuja na marafiki zako?” Inspekta alimuuliza mwanawe Fumo.

“Naam baba leo niko na wenzangu. Kuna jambo la dharura ambalo tunataka kukueleza .” Fumo alisema huku yeye na wenzake wakikaa kwenye makochi sebuleni.

“Haya masikio yangu nimewapa, hebu nielezeni kuna nini?” Inspekta alimuuliza Fumo.

Fumo, Waridi na Shaka wakamweleza inspekta kuhusu kisa cha Rehema. Inspekta aliwasikiliza watoto kwa makini walipomweleza kuhusu kisa cha Rehema. Walipomaliza kuongea alisimama na kutembea sebuleni huku na kule akiwa amezama katika luja la fikra, kisha akawauliza watoto.

“Je, mna ushahidi zaidi kuhusu hili jambo mlilonieleza? Mnajua sisi polisi hatuwezi kuchukua hatua hadi tuwe na ushahidi wa kutosha.” Inspekta aliwaeleza.

“Baba, tunaweza kwenda kwa kina Rehema sasa hivi ujionee mwenyewe.” Fumo alimweleza baba yake. Kabla ya Inspekta kujibu, mlango ulibishwa ghafla na Mzee Pilipili akaingia sebuleni. Mzee Pilipili alikuwa kaiva kwa hasira na macho yake yalikuwa mekundu kama pilipili nyekundu. Mzee Pilipili alishtuka kumwona Inspekta akiwa na watoto wale sebuleni. Fumo na wenzake nao waliduwaa kumwona Mzee Pilipili tena.

“Inspekta! Nimekuja kuwashtaki hawa watoto.” Mzee Pilipili alisema huku akiwaonyesha kina Fumo.

“Enhe! Wamefanya nini?” Inspekta alimuuliza Mzee Pilipili.

“Waeleze mambo ya kuja kwangu bila ya idhini yangu ni makosa makubwa sana. Kama wanataka kumtafuta Rehema waambie wamngojee shuleni.” Mzee Pilipili alisema.

Inspekta alimtazama Mzee Pilipili kutoka utosini hadi miguuni,kisha akaamua kumuuliza maswali.

“ Mbona Rehema hajaenda shule kwa muda wa wiki mbili?”

“Mwanangu Rehema ni mgonjwa.na yuko nyumbani .” Mzee Pilipili alijibu.

“Je, unapanga kumwoza Rehema kesho?” Inspekta alirusha swali lililomshtua Mzee Pilipili.

“Sasa mimi nitamwozaje mwanangu mchanga ? Mbona hawa watoto wananisingizia mimiMzee mzima?” Mzee Pilipili alijibu.

“Je, unajua kuwa nikithibitisha kuwa unataka kumwoza msichana mdogo kinyume na sheria nitakutia mbaroni na kukupeleka kortini?” Inspekta alimwambia Mzee Pilipili.

“Aaah! Inspekta, usifuatilie sana hizi hadithi za watoto. Hawa watakudanganya wakupoteze.” Mzee Pilipili alijibu huku akichekacheka kwa woga.

“Basi nataka sote tuambatane twende kwako ili nimhoji Rehema .” Inspekta alisema.

“Sawa twendeni.” Mzee Pilipili alikubali shingo upande na wote wakaondoka kuelekea kwa kina Rehema.

Walipofika kwa Mzee Pilipili, aliwaingiza hadi katika chumba cha kulala cha Rehema. Rehema alikuwa amelala fofofo. Kando ya kitanda chake kwenye kimeza kidogo kulikuwa na dawa aina nyingi.

“Ooh! Sasa nimethibitisha kuwa Rehema ni mgonjwa. Lakini nitakuja tena jioni akiamka ili niongee naye.” Inspekta alisema kisha akatoka na Fumo, Waridi na Shaka wakarudi kwake.Waliporudi sebuleni kwake, Inspekta aliwaeleza Fumo na wenzake.

“Mkitaka nichukue hatua yoyote nitahitaji ushahidi wa kutosha. Sijaona jambo lolote linaloonyesha kuwa Rehema anaozwa kesho. Mmeona nyote kuwa Rehema ni mgonjwa na alikuwa amelala fofofo.”Fumo na wenzake walitazamana kwa mshangao.

Je, unafikiri watoto wanasema ukweli? Eleza sababu ya jibu lako.